Wednesday 18 September 2013

Uharifu wa kutisha Ngara dhidi ya wafugaji

- Unachochewa na vyombo vya habari
-Wafugaji wanachangia elimu na kulipa kodi lakini hawathaminiwi
-Wanaitwa wahamiaji haramu wakati ni Watanzania
-Ubaguzi na apartheid lazima vikemewe
Kuna dhana iliyojengeka mkoani Kagera kuwa kila mtu mwenye asili ya Rwanda ni mhamiaji haramu na kila mtu mwenye sura ya Kitutsi ni mhamiaji haramu. Waingereza wanasema give a dog a bad name and hang it. Yaani mpe mbwa jina baya kisha mwuue. Hilo ndio linafanyika hasa katika wilaya ya Ngara mkoa wa Kagera kwani raia wema wanaitwa wahamiaji haramu kisha wanatendewa dhuluma kubwa, huku vyombo vya habari vikifanya kazi ya uchochezi.
Naandika makala hii baada ya kusoma makala kwenye Raia Mwema iliyoandikwa na Ezekiel Kamwaga (Raia Mwema Toleo namba 316, Sept. 18-24). Katika makala hiyo yenye kichwa cha habari: “Rafu uhamiaji haramu”, ametengeneza picha kuwa watu wa Kigoma wanaonewa, huku wahamiaji haramu kutoka Rwanda wakikingiwa kifua.
Habari hiyo imeandikwa maksudi kwani ya wana Kigoma imeandikwa vizuri bila ‘omission’, yaani kila kuacha kitu, mwandishi amefanya utafiti na kupata vielelezo. Kuhusu Mtanzania mwenye asili ya Rwanda kule Ngara, mwandishi hakujisumbua kutafuta vielelezo, amempa mtuhumiwa paragraph moja kukanusha ili kuonyesha kuwa haikuwa ya upande mmoja. Na kwa kutumia mfano wa mfugaji mmoja, akajumuisha kuwa watu wenye asili ya Rwanda wenye mali hawakuguswa, na kudai kuwa operation Kimbunga imewalenga vibarua na watu wa chini.
Kufuatia makala hii, huenda mfugaji huyu akavamiwa na watu wa Ngara na mifugo yake kukatwakatwa akituhumiwa kuwa mhamiaji haramu anayetoa rushwa kwa viongozi ili aishi kwa kuharibu mazingira, kuua tembo na kulisha kwenye mashamba ya watu, kama alivyotuhumiwa kwenye makala ya Kamwaga.
Kuna mifano hai ya namna vyombo vya habari vinavyochochea uhalifu Ngara. Tarehe 31 Mei mwaka 2011 Ngara kulitokea uhalifu wa kutisha uliosababisha vifo vya watu saba na kujeruhiwa vibaya ngo’mbe 400, ambao baadae walichinjwa na kuliwa na hao waliowajeruhi. Haya yote yalichochewa na vyombo vya habari.
Ngara kuna kundi la watu ambao ni wawindaji. Na kila walipokuwa wanawinda na kukosa mnyama, walikuwa wanapita mazizini na kuua ndama na kwenda nao kama nyama. Siku moja, mfugaji mmoja  katika pori la Rubagabaga kijiji cha Murbaga, tarafa ya Mursagamba wilayani Ngara akamwambia mchungaji wake kuwa akae zizini mchana na mtu yoyete atakayeua ndama apambane nae.
Ilikuwa mida ya saa tano hivi, na wawindaji wakapita na kuua ndama wawili. Yule mchungaji, ambaye ni mzaliwa wa Ngara, akawashambulia kwa mikuki na kuua wawindaji sita katika vita hiyo. Mmoja akakimbia na kuelekea vijijini.
Kesho yake ‘operation’ ikaanza. Wakulima wakaua kijana mmoja mfugaji kwa kutenganisha kichwa chake na kiwiliwili, wakajeruhi ng’ombe 400 ambao walikufa kwa maumivu na nyama yao kuliwa na wana vijiji.
Vyombo vya habari vikapamba vichwa vya habari: “Wafugaji haramu wawaua Watanzania Ngara”, “wahamiaji haramu wakingiwa kifua na watendaji serikalini” n.k.
Tangu wakati huo mpaka leo tumekuwa tukipata habari za upande mmoja kuonyesha kuwa wahamiaji haramu Wanyarwanda wameingia Tanzania na makundi makubwa ya ng’ombe na wanaishi kwa kutoa rushwa na kuvuruga maisha ya watu wa Ngara na kuharibu mazingira. Hali hii imewapa wakazi wa Ngara kiburi cha kufanya uharifu wanapojisikia, wanakatakata mifugo mara kwa mara, wanavamia mazizi na kuswaga mifugo.
Hali hii inaenea hata Karagwe na imetokea kata ya Nyakasimbi, wilaya ya Karagwe ambapo mwezi Mei mwaka huu mtu mmoja mwenye asili ya Rwanda alinunua ardhi na wana kijiji kisha akaizungushia uzio. Wanakijiji wakacharuka na kuingia zizini kwake na kuswaga mifugo, kufyeka migomba yake na kuharibu nyumba, huku wakimtuhumu kuwa mhamiaji haramu amevamia ardhi yao.
Kutokana na uhalifu huo, polisi mkoani kagera iliwakamata baadhi ya watu kwa wizi wa kutumia silaha, kwani waliiba mifugo wakiwa na silaha. Kilichofuatia, Mbunge akaitisha mkutano wa kijiji, wakamlalamikia, nae kwa kuwasikiliza wapiga kura wake, akamwomba waziri wa mambo ya Ndani Emmanuel Nchimbi aingilie kati.
Dr Nchimbi aliunda tume ambayo ilipendekeza RCO wa mkoa wa Kagera Peter Matagi afukuzwe kazi kwa kuwabambikizia kesi hao wahalifu walioingia zizini na silaha na kuswaga mifugo kinyume cha sheria.

Ukweli kuhusu wafugaji wa Ngara
Wafugaji walioko Ngara wametokea Muleba na karagwe, kwani kwa watu wanaoijua Rwanda, haina ardhi ya kutosha kufugia mifugo mingi. Kwa waliowahi kwenda huko bila shaka waliona kuwa kila familia ina ng’ombe mmoja wa kisasa, hakuna ardhi. Hivyo wanaosema mifugo inatoka Rwanda wanataka kueneza propaganda ya kupelekea watu kudhulumiwa.
Pili si kila mtu mwenye asili ya Rwanda ni mhamiaji haramu. Mwaka 1980, shirika la UNHCR na serikali ya Tanzania zilifanya makubaliano ya kuwapa uraia wakimbizi wa Kitutsi kutoka Rwanda. Maafisa Uhamiaji na UNHCR walipita kwenye makambi ya Muyenzi (Ngara), Kimuli (Karagwe) na Mwese (Rukwa) wakiandikisha wakimbizi. Zaidi ya wakimbizi 30,000 walipewa uraia wa Tanzania.
Sheria za uraia za mwaka 1962, 1972 na 1995 zinasema mtu akizaliwa na raia mmoja Mtanzania basi yeye ni Mtanzania. Kwahiyo Wanyarwanda waliozaliwa baada ya mwaka 80 wakati wazazi wao walishapewa uraia, ni raia, ni sawa na watu wenye asili ya Asia ambao wanaishi Dar es Salaam bila kubughudhiwa ni kwamba wazazi wao walipewa uraia zamani.
Mwandishi Kamwaga aliangukia kwenye mtego wa kuwaita Wanyarwanda wote wahamiaji haramu, labda angejaribu kumwomba yule ‘kigogo’ mfugaji cheti chake cha uraia, au hati yoyote ingesaidia kujua ukweli.
Lakini sikustaajabu kwani nia ya Kamwaga haikuwa kutafuta ukweli bali kueneza propaganda za watu wanaofaidika na dhuluma dhidi ya wafugaji na kusema kuwa watu wa asili ya Rwanda waliobaki walipaswa kuswagwa bila kujali kuwa ni raia.
ina uhakika asilimia 100 kuwa hao wafugaji waliopewa majina ya uhamiaji haramu, waharibifu wa mazingira na wauaji wa Tembo watashughiulikiwa na wanakijiji wa Ngara ambao wamejijengea utamaduni wa uharifu.
Na nimeshangaa kusoma kuwa wahamiaji haramu walioondoka ni vibarua tu. Mwandishi amekwepa kwa makusudi kusema yaliyowakuta wafugaji wa Ngara katika operation hii. Wengi wao walikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi Benaco na mifugo yao kufungiwa kwenye mnada wa Kafuha.
Mifugo ilikaa Kafuha kwa siku nne bila maji na majani, baadhi ya ng’ombe wakatoroka na kuingia kwenye mashamba ya watu na jumla ya ng’ombe 80 walikatwakatwa miguu, na wengine kama 200 waliibwa na kupakiwa malori na kupelekwa Kahama huku wenye mali wakiwa rumande wanahojiwa.
Walioachiwa ni wenye vyeti vya uraia, wasio na vyeti waliswagwa. Na isingekuwa rahisi kutoa rushwa kwani operation inahusisha watendaji wa idara zote za ulinzi na usalama. Lakini haya hayakusemwa, bali Kamwaga anaimba kuwa wahamiaji haramu wenye pesa wameachwa. Tusubiri matokeo ya kalamu ya Kamwaga.
Jkalisa79@gmail.com

No comments:

Post a Comment